JINA la winga Sunday Juma, si geni masikioni mwa wapenzi wa soka nchini hasa wale wa klabu ya Simba maarufu Wekundu wa Msimbazi, kwani ameichezea timu hiyo kwa mafanikio makubwa kwa kipindi cha takribani miaka 10 kuanzia 1980 hadi 1990.
Sunday pamoja na kuichezea klabu ya Simba kwa mafanikio makubwa, pia amezichezea klabu kadhaa zikiwemo Kibo ya Moshi, timu za mikoa ya Kilimanjaro ‘Kilimanjaro Stars’ na Dar es Salaam maarufu Mzizima United pamoja na timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
Nyota huyo mwenye umbo fupi kiasi, hivi sasa haonekani viwanjani kwa maana ya kucheza soka kwa sababu alistaafu kucheza mchezo huu unaopendwa zaidi duniani kote mwishoni mwa mwaka 1990, wakati huo akiichezea timu ya Simba yenye makao yake makuu Kariakoo Mtaa wa Msimbazi.
Licha ya Sunday kustaafu kucheza soka la ushindani, lakini bado anaufuatilia kwa kuangalia michezo ya ligi kuu na pia kufuatilia katika runinga mechi za soka zinazochezwa Ulaya na kutoa maoni yake kwa vijana wanaochipukia, kwa sababu yeye ni mdau mkubwa wa mchezo huu.
Hivi karibuni SPOTI KIKI lilikutana na mstaafu huyo ambaye hivi sasa ni mjasiriamali anayemiliki duka la vifaa vya urembo na vipodozi lililopo Kariakoo, jijini Dar es Salaam na kufanya naye mahojiano kuhusiana na masuala ya soka kipindi anacheza soka ya ushindani miaka ya nyuma na yanayojiri hivi sasa.
Sunday pamoja na mambo mengine anatoa ushauri kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwapa kipaumbele makocha wazawa wenye uwezo wa kufundisha timu yetu ya Taifa na kuondokana na kasumba iliyojengeka ya kutafuta makocha kutoka nje ya nchi ambao baadhi yao hawana uwezo.
“Huu ni wakati mwafaka kwa TFF kulipa umuhimu suala hili na kuanza kuwatumia makocha wazawa wenye uwezo na kuachana na makocha wa kigeni waliotufikisha hapa tulipo.
“Wapenzi wa soka wamekuwa wakishuhudia baadhi ya makocha kutoka nje hawana jipya, kwani viwango vyao au madaraja waliyonayo hayatofautiani na walimu wazawa tulionao na wengine inawezekana wako juu kuliko wageni.
“Ni vyema tukaanza kuwatumia makocha wazawa wenye uwezo ili kuondoa ile dhana ya Tanzania kuitwa kichwa cha mwendawazimu, kwani baadhi ya hao wanaotoka nje ndio wamesababisha kiwango cha soka letu kuzidi kushuka siku hadi siku.
“Mfano mzuri tumeanza kuuona kwani baada ya kuchaguliwa kocha mzawa kufundisha timu yetu ya Taifa, Charles Mkwasa, kwa kiasi fulani matunda yameanza kuonekana ukilinganisha na makocha wa kigeni tuliokuwa nao kipindi cha nyuma.
“Kuwatumia makocha wazawa wenye uwezo kuna faida nyingi ikiwemo moja kubwa ya walimu wa hapa nchini kuwafahamu vizuri wachezaji wetu kuanzia tabia na mazingira wanayoishi.
“Pia wachezaji wetu wanawaelewa makocha wazawa kwa urahisi zaidi kulinganisha na makocha kutoka nje ambao baadhi yao lugha wanayotumia ni ngumu kueleweka, hivyo ni vyema kuachana nao kabisa ili tuwape nafasi wazawa,” anasema.
Sunday anamalizia kwa kuwashauri wachezaji wa sasa akiwataka kujituma, kucheza kwa bidii na kuachana na starehe ambazo hazina msingi ili waweze kuinua viwango vyao vya soka.
“Kama wachezaji wa sasa wanataka kuinua viwango vyao vya soka ni vyema wakajituma na kucheza kwa bidii na kuweka kando mambo ya starehe kama vile kunywa pombe kwani starehe ni sumu kubwa kwa anayetaka kusonga mbele kisoka.
“Hivi sasa mchezo wa soka unalipa sana  ukilinganisha na wakati sisi tulipokuwa tunacheza, kwani wakati huo kulikuwa hakuana fedha kama sasa hivi ambapo wachezaji wanasajiliwa kwa fedha nyingi na kupata marupurupu mengi.
“Hivyo kama wachezaji wa sasa wanatakiwa kusonga mbele kwenye soka na kufanya maisha yao kuwa bora, wanatakiwa kucheza kwa bidii, kujituma na pia kuuchukulia mchezo huu kama ajira kama zilivyo nyingine,” anasisitiza Sunday.
Huyo ndiye Sunday Juma winga machachari aliyetamba akiwa na klabu za Simba, Kibo ya Moshi, timu za mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Taifa Stars.
Share To:
Magpress

MagPress

Vestibulum bibendum felis sit amet dolor auctor molestie. In dignissim eget nibh id dapibus. Fusce et suscipit orci. Aliquam sit amet urna lorem. Duis eu imperdiet nunc, non imperdiet libero.

0 comments so far,add yours