NAIBU Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel, kuwakamata watu wote wanaofanya mapenzi na wanafunzi wa shule za msingi.
Jafo aliyasema hayo juzi wilayani hapa, wakati wa ziara yake ya kutembelea Shule ya Sekondari Mnyuzi na Shule za Msingi za Kilimani na Gereza.
Akiwa kwenye shule hizo, Jafo alikagua na kuridhishwa na thamani ya fedha zilizotumika katika ukarabati wa shule hizo.
Pamoja na hayo, aliwataka viongozi wa wilaya hiyo kutowafumbia macho watu wanaoharibu malengo ya wanafunzi kwa kufanya nao mapenzi. “Mheshimiwa mkuu wa wilaya, lipo tatizo la wanafunzi wa kike wanaopewa mimba na baadhi ya wanaume. “Wanaume hao wakamateni, muwaweke ndani kwa sababu hatuwezi kuvumilia vitendo vya aina hiyo kwenye jamii yetu. “Haiingii akilini kuona wazazi na Serikali wanatumia gharama kubwa kuwasomesha watoto, halafu jitihada hizo zinakwamishwa na waovu fulani, hatuwezi kukubali. “Sisi kama Serikali, tutahakikisha suala hilo tunalifanyia kazi kwa mapana yake ili liweze kuondoka kwenye jamii kwa sababu tunataka wanafunzi wa kike wasome bila vikwazo,” alisema Jafo.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel, alimuahidi Jafo kwamba, atafanyia kazi maagizo hayo ili wanafunzi wa kike wasikatishwe masomo yao.
0 comments so far,add yours