BEIJING, CHINA
SIKU mbili tu baada ya Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, kukaririwa akisema amezungumza na sehemu kubwa ya viongozi wa dunia isipokuwa Rais wa China, Xi Jinping, hatimaye wawili hao wamezungumza.
Rais Jinping alimpigia simu Trump kumpongeza na kusisitiza kuwa ushirikiano baina yao ni ‘chaguo pekee’ la uhusiano wa mataifa yao, si vita ya kibiashara.
“Rais mteule Donald Trump na Rais wa China Xi Jinping walionyeshana heshima katika mazungumzo yao kwa njia ya simu Jumapili usiku,” ilisema Ofisi ya Mpito ya Trump mapema jana.
Katika taarifa yake, ofisi hiyo ilisema kuwa Trump alimshukuru Jinping kwa pongezi zake baada ya kushinda uchaguzi wa urais uliofanyika Jumanne iliyopita dhidi ya mpinzani wake wa Chama cha Democrat, Hillary Clinton.
“Wakati wa mazungumzo, viongozi hao walionyesha hali ya kuheshimiana na Trump alieleza kuwa anaamini watakuwa na uhusiano imara kwa manufaa ya nchi zao,” ilisema taarifa ya ofisi hiyo.
Hata hivyo, gazeti linalomilikiwa na Serikali la Global Times, limeripoti kuwa Jinping alimwambia mfanyabiashara huyo bilionea kwamba ushirikiano baina yao ni chaguo pekee kwa uhusiano wa mataifa hayo mawili.
Lilisema kuwa utakuwa ni ‘utoto na ujinga’ iwapo Trump atazindua vita ya kibiashara dhidi ya China.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, iwapo hilo litatokea, China pamoja na mambo mengine itasitisha ununuzi wa bidhaa za Marekani, ikiwamo ndege aina ya Boeing, simu aina ya iPhones na magari.
Trump alikuwa akiishambulia China wakati wa kipindi chote cha kampeni zake za uchaguzi, akiapa kuziwekea ushuru wa asilimia 45 bidhaa zao na kushughulikia kile alichokiita hujuma za sarafu ya nchi hiyo katika siku yake ya kwanza madarakani.
Agosti mwaka huu, Trump aliituhumu Beijing kwa wizi mkubwa katika historia ya dunia.
Hivyo, ushindi wake ulizua wasiwasi kuhusu uhusiano wa mataifa hayo yanayoongoza kwa ukubwa wa uchumi duniani.
Awali Ijumaa iliyopita, Trump aliliambia Jarida la Wall Street kuwa amezungumza nao au kuwasikia viongozi wengi duniani isipokuwa Jinping.
Kauli hiyo ilifuta zile zilizoripotiwa awali kuwa Jinping alikuwa miongoni mwa viongozi waliompongeza Trump wakati alipotangazwa kushinda urais Jumatano iliyopita.
Msemaji wa Trump, Hope Hicks, aliliambia Shirika la Habari la CNN badaye siku hiyo kuwa kilichoandikwa na Wall Street Journal ni cha kweli.
Katika mazungumzo yao ya juzi usiku, wawili hao pia walikubaliana kukutana hivi karibuni na kubadilishana mawazo na mitazamo katika maeneo ya wasiwasi baina ya pande hizo mbili.
Share To:
Magpress

MagPress

Vestibulum bibendum felis sit amet dolor auctor molestie. In dignissim eget nibh id dapibus. Fusce et suscipit orci. Aliquam sit amet urna lorem. Duis eu imperdiet nunc, non imperdiet libero.

0 comments so far,add yours