Chama cha demokrasia na maendeleo ( CHADEMA ), kimesema hakuna sababu
ya wananchi wa kabila la wasukuma katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu
kuendelea kuwa maskini, wakati almasi peke yake iliyoanza kuchimbwa
tangu mwaka 1942 katika mgodi wa mwadui, ingeweza kuboresha maisha yao
mbali na wingi wa mifugo pamoja na uzalishaji wa zao la pamba na kusema
wakati umefika kwa wananchi wa kabila hilo kutumia raslimali walizonazo
katika kupiga vita umaskini.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa lagangabilili
wilayani itilima, mwenyekiti wa taifa wa chadema Mh. Freeman Mbowe
amesema kwamba licha ya mikoa ya usukumani kusifika kwa uzalishaji wa
pamba iliyopelekea kujengwa kwa viwanda vitano vya nguo ambavyo ni
pamoja na Mwatex,Mutex,Kilitex,Kunguratex na urafiki wakati wa enzi za
mwalimu Julius Nyerere, lakini amedai kuwa bado wasukuma ni maskini
ukilinganisha na makabila mengine nchini kwa miaka 53 baada ya uhuru.
Mh. Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni
akizungumzia mpango wa Chadema unaojulikana kama ‘FTP 200’ unaokusudia
kuwafanya vijana wa kitanzania kuwa wazalendo kwa nchi yao katika
kuwaepusha na vikundi vya kihalifu kama vile panya Road na Mbwa Mwitu
kwa kusaidiana na jeshi la polisi kufichua vitendo vya uhalifu,amesema
pindi ukikamilika mwezi juni mwaka huu utawafikia vijana zaidi ya
milioni moja nchi nzima ambao wanaishi bila ajira rasmi kupata stadi za
ujasiriamali,Elimu ya afya,nidhamu na kupiga vita Rushwa katika jamii.
Katika hatua nyingine wazee wa kabila la kisukuma wilayani humo
wamemsimika mwenyekiti huyo wa taifa Chadema na mbunge wa jimbo la hai
Mh.Freeman Mbowe kuwa Chifu wa kabila hilo baada ya kumvisha mgolole
pamoja na kumkabidhi mkuki, ngao na kibuyu – huku wazee hao wakimpatia
jina la mayengo na kutaka vyombo vya dola kutenda haki kwa vyama vyote
vitakavyoshiriki katika uchaguzi mkuu.
0 comments so far,add yours