Jeshi la polisi mkoani Simiyu
linamshikilia Shabani Ernest 22 mkazi wa kijiji cha Kitongo wilayani
Magu kwa tuhuma za kukutwa na noti bandia.
Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa polisi wa mkoa wa
Simiyu kamishina msaidizi mwandamizi,Charles Mkumbo amesema kuwa
mtuhumiwa huyo ni karani wa kampuni ya kununua pamba ya Olam ya wilayani
Bunda mkoani Mara na kwamba alikamatwa juzi katika kijiji cha Mwanunui
kilichoko katika kata ya Mwarushu wilayani Itirima ambapo ndipo
alipokuwa akinunulia pamba.
kamanda mkumbo amesema kukamatwa kwa karani huyo kulitokana na
kuwalipa baadhi ya wakulima pesa bandia ambao waliweza kuzingundua na
kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji.
Amefafanua kuwa baada ya kukaguliwa alikutwa na noti za shilingi
elfu kumi zipatazo 40 ambazo kama zingekuwa harari zingekuwa na thamani
ya laki nne ambazo alikuwa akizitumia kuwalipa wakulima wa zao la pamba.
Aidha kamanda huyo ametoa wito kwa wananchi wawe macho hususani
wakulima wanaouza mazao yao kipindi hiki cha msimu wa pamba kutokana na
kuzagaa kwa noti hizo.
Pia amewaonya wafanyabiashara wanaonunua mazao ya biashara mkoani
humo kuwa waaminifu na kuacha kujihusisha na biashara ya noti bandia kwa
kuwalipa wakulima na kwamba jeshi hilo halitamufumbia macho
mfanyabiashara wa kampuni yeyote ile atakayebainika.
0 comments so far,add yours