NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alimdhibiti Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko (Chadema), kwa kumtaka asisome maelezo yasiyohusiana na Muswada wa Sheria ya Wanataaluma wa Kemia ya Mwaka 2016.
Tukio hilo limetokea wakati bado kuna kumbukumbu za wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia baadhi ya vikao vya Mkutano wa Bunge la Bajeti vilivyoanza Aprili hadi Julai, mwaka huu vilivyoongozwa na Dk. Tulia kutokana na kile walichodai kuwa hawakuridhishwa na mwenendo wa utendaji wake.
Tukio hilo lilitokea bungeni jana baada ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kusoma kwa mara ya pili muswada huo baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Katika tukio hilo, Matiko, aliyekuwa akisoma maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu muswada huo, alianza kuwashukuru Watanzania kwa ushirikiano walioutoa wakati wa maandalizi ya maandamano yaliyoandaliwa na Chadema na kupewa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).
Pia, Matiko alivishutumu vyombo vya ulinzi kwa kile alichosema vilishiriki kuwakamata wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wakati wa maandalizi ya maandamano hayo yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Septemba mosi, mwaka huu kabla hayajaahirishwa hadi Oktoba mosi, mwaka huu.
Wakati mbunge huyo akiendelea kusoma, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu, Dk. Abdallah Possi, alisimama na kuomba utaratibu huku akieleza jinsi mbunge huyo anavyosoma mambo yasiyokuwa na uhusiano na muswada husika.
Baada ya maelezo hayo, Dk. Tulia, alisimama na kuungana na Dk. Possi na kumtaka Matiko ajielekeze katika muswada ili asivunje kanuni za Bunge.
“Mheshimiwa Matiko, kanuni ya 86 (6,7,8) inazuia mbunge kutoka nje ya hoja, kwa hiyo nakuomba ujikite kwenye muswada kwa mujibu wa kanuni,” alisema Dk. Tulia.
Pia alimtaka Matiko aendelee kutoa maoni ya kambi hiyo ambapo mbunge huyo alisema ana haki ya kuyasema kwa kuwa ni mbunge wa kuchaguliwa na kwamba maelezo yaliyokuwa yakilalamikiwa ni utangulizi wa hotuba ya upinzani na baada ya hapo aliendelea tena kuvishutumu vyombo vya dola.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Possi, alisimama tena na kuomba utaratibu akisisitiza matumizi ya kanuni hiyo ya 86.
Kauli hiyo ilimfanya Dk. Tulia asimame tena na kumtaka Matiko asiendelee kuvunja kanuni kwa kuwa zilitungwa ili kuwaongoza wabunge.
Wakati anasimama, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alikuwa amesimama na kupaza sauti akimuunga mkono Matiko jambo lililomfanya Dk. Tulia amwamuru kukaa chini.
“Mheshimiwa Halima Mdee, kaa chini, hapa tunafuata kanuni, nakuomba hata wewe mheshimiwa Matiko, ujikite kwenye hoja, nakuomba tafadhali usivunje kanuni,” alisisitiza Dk. Tulia.
Baada ya maelekezo hayo, Matiko, aliamua kutoendelea na maneno yaliyokuwa yakilalamikiwa na kujikita kwenye hoja.
“Sasa najikita katika hoja, lakini message sent, nakushauri pia ukipata muda, ukasome kitabu kinaitwa The great dictator,” alisema Matiko huku akiendelea kuwasilisha maoni ya kambi ya upinzani.
Pamoja na Matiko, awali Dk. Tulia alimzuia pia Mbunge wa Siha, Godwin Mollel (Chadema), kusoma maelezo yasiyohusiana na Muswada wa Sheria ya Uanzishwaji wa Baraza la Wanataaluma wa Kemia wa mwaka 2016 uliosomwa kwa mara ya pili na Ummy.
Share To:
Magpress

MagPress

Vestibulum bibendum felis sit amet dolor auctor molestie. In dignissim eget nibh id dapibus. Fusce et suscipit orci. Aliquam sit amet urna lorem. Duis eu imperdiet nunc, non imperdiet libero.

0 comments so far,add yours