Wawekezaji wengi kutoka nje ya nchi wameanza kuonyesha nia ya kutaka kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya Sukari nchini baada ya rais John Pombe Magufuli kuzuia uagizaji wa sukari toka nje ili kuvilinda viwanda vya ndani.
Rais wa chama cha wanasayansi na wataalam wa Sukari na Miwa nchini (TSSCT) Mhandisi Nestory Rwechungura amesema hayo katika mkutano mkuu maalum wa wataalam hao kutoka ndani na nje ya nchi wanaokutana mjini Moshi kuweka mikakati ya nchi kujitosheleza kwa Sukari.
Mhandisi Rwechungura amesema, mikakati pia imeanza ya kuvipanua viwanda vya ndani ili kuziba pengo la uagizaji wa Sukari toka nje ambavyo vitasaidia kupanua ajira kwa vijana, kuongeza wataalam wanaomaliza vyuo vikuu na pato la taifa.
Hata hivyo wataalam hao wamesema, wazalishaji wa Sukari nchini wakiwemo wakulima wadogo wana changamoto ya uzalishaji kutokana na kupanda kwa gharama ya teknolojia na kuifanya Tanzania kuwa na gharama kubwa ya uzalishaji katika hekta moja ikilinganishwa na nchi za Brazil, Kenya, Uganda na Malawi.
Akifungua mkutano huo mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Bw Said Meck Sadiki katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa wilaya ya Moshi Bw Novatus Makunga amewapongeza wazalishaji wa Sukari kwa mikakati ya upanuzi wa viwanda ambao pia utawasaidia wakulima wadogo kupata soko la Miwa.
0 comments so far,add yours