Kamati ya bunge ya hesabu za serikali PAC imebaini upotevu wa fedha
zaidi ya shilingi bilioni 1.5 za mamlaka ya usimamizi wa bandari TPA
ambazo zimetumika lakini nyaraka zake hazionekani huku ikiuagiza uongozi
wa mamlaka hiyo kuhakikisha fedha zote za nyongeza ya posho za safari
walizolipwa watumishi tangu mwaka 2011 kabla msajili wa hazina
hajathibitisha zinarudishwa.
Mwenyekiti wa kamati ya PAC Mh Zitto Kabwe ametoa agizo hilo wakati
kamati yake ilipokutana na bodi na uongozi wa TPA baada ya kukagua
vitabu vyake vya mahesabu ambapo amesema licha ya kiwango cha posho
zilizolipwa kuwa kikubwa lakini waliharakisha kujilipa kabla msajili wa
hazina hajathibitisha ambapo afisa wa ngazi ya juu alilipwa shilingi
laki tano kwa siku kwa safari ya ndani ya nchi na ya nje ya nchi dola za
kimarekani mia nane.
Akizungumzia suala la ukosefu wa nyaraka za fedha ambazo tayari
zimeshatumika makamu mwenyekiti wa PAS Mh.Deo Philikonjombe amesema
tatizo hilo limekuwa sugu kwa taasisi mbalimbali za serikali hali
inayoashiria kuwa kuna baadhi ya wakurugenzi na watumishi wanafuja fedha
za umma kinyume na taratibu na wanapobanwa wanapeleka nyaraka ambazo
wakati mwingine ni za kufoji.
Kaimu mkurugenzi mkuu wa TPA na mhasibu wake mbali na kukiri
upotevu wa nyaraka hizo wamedai kuwa tatizo hilo limetokana na uhifadhi
wa nyaraka ambao hadi leo nyaraka nyingi za TPA zinahifadhiwa kwenye
karatasi na kuiahidi kamati hiyo kuwa wataziwasilisha mwisho wa mwezi wa
mwezi febuari mwaka huu hali iliyozua maswali mengi kwa wajumbe wa
kamati hiyo kuwa watazipata wapi kama kipindi chote hicho hazijaonekana.
0 comments so far,add yours