Mfanyabiashara wa Tanzania Bw. Patrick Ngowi ni miongoni mwa
wafanyabiashara 100 walioingia fainali za kuwania tuzo ya mfanyabiashara
bora kijana wa mwaka barani afrika, zitakazofanyika Afrika kusini
novemba 14 mwaka huu.
Akiwa na umri wa miaka 28, Bw. Patrick Ngowi ambaye ni mwenyekiti
wa kampuni ya Helvetic Group, inayotengeneza vifaa vya umeme wa jua,
ametangazwa kuwa ni miongoni mwa wafanyabiashara 100 walio na umri
usiozidi miaka 40, waliofanikiwa na wanaotarajiwa kufanya vizuri zaidi
miaka ijayo.
Katika orodha hiyo wapo watanzania wengine 9, ikiashiria kuwa kuna
uwezekano kuwa asilimia 10 ya wafanyabiashara wakubwa wa miaka ijayo
barani Afrika, watakuwa ni watanzania.
Kwa mujibu wa rais wa taasisi ya Choiseul Bw. Pascal Larot, kila
mwaka taasisi yake hufanya utafiti wa kusaka na kuorodhesha katika
madaraja wafanyabiashara vijana wanaochipukia kiuchumi, wenye umri
usiozidi miaka 40, ambao watashiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa
bara hili miaka ya hivi karibuni.
Hivi karibuni chaneli ya televisheni ya mambo ya fedha na biashara -
CNBC ilimtunuku Bw. Patrick Ngowi tuzo ya mwaka ya mfanyabiashara
kijana wa Afrika Mashariki, katika hafla iliyofanyika jijini nairobi,
kenya, ambayo mwenyekiti mtendaji wa IPP Dr Reginald Mengi pia
alitunukiwa tuzo ya mfanyabiashara bora wa mwaka Afrika Mashariki.
0 comments so far,add yours