Baadhi ya Wafanyabiashara wa kati Mjini Morogoro wamefunga maduka yao kwa hofu ya kufungiwa na Mamlaka ya mapato nchini TRA na kutozwa mamilioni ya fedha kama faini kutokana na kutokuwa na mashine za risiti za kielektroniki za (EFD) ,wakidai hatua hizo zimeanza kuchukuliwa jijini Dar es salaam, huku bado mazungumzo kati ya TRA na wafanyabiashara yakiwa bado hayajakamilika.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa kati mjini
Morogoro, Ali Mamba amesema mgomo huo hauhusiani na matumizi ya mashine
hizo bali mfumo mzima wa ulipaji wa kodi kwa wafanyabiashara ambao
pamoja na kushawishiwa kuachana na mgomo huo, wamedaai kuchukua uamuzi
huo kwa kutowaamini viongozi wao katika mazungumzo yaliyokuwa
yakiendelea baina yao na TRA, kwa kushuhudia mamlaka hiyo ikianza
kuwafungia wafanyabiashara jijini Dar es salaam.
Kufungwa huko amesema kunakwenda sambamba na
masharti magumu ikiwemo kutakiwa kulipa faini ya sh milioni tatu,
kununua mashine kwa laki sita na shilingi elfu themanini ya kufuli
linalotumika kufungia eneo husika linalofungiwa.
Nao wafanyabiashara wanaosambaza bidhaa katika
maduka mbalimbali, walieleza kuathiriwa na mgomo huo na kwamba pamoja na
kutumia mashine husika, bado mtandao wake ni wa tabu, hivyo TRA badala
ya kutaka wafanyabiashara watumie mashine ni vyema ikaangalia pia na
changamoto zilizopo kwenye mfumo huo kabla ya kuhimiza matumizi.
Meneja wa TRA mkoa wa Morogoro Kilomba Kanse,
alikataa kuzungumzia hali hiyo kwa madai tayari Kamishna mkuu wa
mamlaka hiyo, Risherd Bade,alishazungumza na vyombo vya habari kuhusiana
na mashine hizo.
Akinukuliwa na vyombo vya habari, Kamishna Mkuu wa
Tra, Risherd Bade,mbali na kuzungumzia umuhimu wa uanzishwaji wa
mashine za EFD, na kuwahimiza wananchi kudai risiti sahihi kwa kiwango
cha fedha wanachotoa wanunuapo bidhaa, amewaonya wanaohamasisha,
kutishia au kutumia njia yoyote kuwarubuni wengine wasitumie mashine
hizo ama kufunga biashara zao waache mara moja, vinginevyo sheria
itachukua mkondo wake.
0 comments so far,add yours