*Picha zinaonyesha jinsi RPC Iringa alivyoshuhudia tukio
*Zinaonyesha baada ya Mwangosi kuuawa, polisi walilaumiana
*Waandishi wa habari, viongozi wa Chadema waangua vilio
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeonyesha picha za mnato na video zinazoonyesha jinsi Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Television cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, alivyouawa.

Picha hizo zilionyeshwa jana jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichohudhuriwa pia na waandishi wa habari. Kikao hicho cha Kamati Kuu kilikuwa ni cha dharura na kilifunguliwa na kuongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.



Wakati picha hizo zikionyeshwa wazi wazi, viongozi wa CHADEMA na waandishi wa habari, walishindwa kujizuia kwani baadhi yao walijikuta wakiangua vilio wakionyesha kusikitishwa na jinsi Mwangosi alivyouawa.

Katika tukio hilo, Mbowe ni kati ya waliolia na ilifika wakati akanyanyuka kutoka meza kuu na kwenda nje ya ukumbi, ili asiendelee kushuhudia Mwangosi alivyouawa.

Wakati picha hizo zikionyeshwa kwa zaidi ya masaa mawili, askari polisi walioshiriki kumuua Mwangosi walionekana wazi wazi na pia Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alionekana pia eneo la tukio akishuhudia Mwangosi akiuawa.

Kwa mujibu wa picha hizo, mwandishi wa habari aliyeanza kukamatwa na askari polisi na kupata kipigo ni Godfrey Mushi wa Gazeti la Nipashe.

Picha hizo za video zilionyesha kuwa, baada ya Mushi kukamatwa, Mwangosi alikwenda kumuokoa mwenzake huyo na alipofika eneo la tukio, askari hao walianza kumpiga na hatimaye kumuua mbele ya Kamanda Kamuhanda.

Picha hizo zinaonyesha kuwa, kabla Mwangosi hajauawa, polisi mmoja alipitisha bunduki yake miguuni kwa polisi mwenzake kisha Mwangosi akauawa.
Share To:
Magpress

MagPress

Vestibulum bibendum felis sit amet dolor auctor molestie. In dignissim eget nibh id dapibus. Fusce et suscipit orci. Aliquam sit amet urna lorem. Duis eu imperdiet nunc, non imperdiet libero.

0 comments so far,add yours