IKIWA imepita mwezi mmoja tangu majaji wawili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuacha kazi kwa wakati mmoja  na kuibua mjadala, jaji mwingine amejiuzulu wadhifa huo.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi na Mawasiliano ya Rais Ikulu jana ilieleza kuwa Rais Dk. John Magufuli ameridhia ombi la Jaji wa Mahakama Kuu, Mwendwa Judith Malecela kujiuzulu wadhifa wake.

Majaji wengine waliojiuzulu ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania,  Jaji Aloysius Mujulizi na mwenzake Upendo Msuya ambao ombi la kujiuzulu kwao liliridhiwa na Rais Magufuli Mei 16, mwaka huu.
Jaji Mujilizi alikubwa na tuhuma za kuhusishwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow kwa kupewa fedha, huku Jaji Upendo ikielezwa kuwa ni mgonjwa.
“Rais Magufuli ameridhia kujiuzulu kwa Mheshimiwa  Mwendwa Judith Malecela kuanzia leo (Juni 20, 2017),” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu.
Chanzo kingine cha habari kililieleza MTANZANIA kuwa tangu alipoteuliwa mwaka 2010 na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, jaji huyo hajawahi kusikika wala katika shughuli zake za ujaji.
Taarifa hizo zilielezwa kuwa jaji huyo wakati wote alikuwa akisumbuliwa na maradhi hali iliyomfanya ashindwe kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa utaratibu.
“Tangu alipoteuliwa Jaji Mwendwa, amekuwa akisumbuliwa na maradhi hali iiliyokuwa ikimfanya ashindwe kutekeleza majukumu yake. Nafikiri kwa hali hiyo ndiyo huenda ni sababu ya yeye kuamua kuomba kujiuzulu wadhifa wake,” alisema mtoa taarifa huyo.
Mbali na majaji hao Mei 16, mwaka huu pia Rais Magufuli aliridhia kuacha kazi kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki, huku kilichowafanya kuacha kazi kikiwa hakijaelezwa.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa siasa walihusisha kuomba kuacha kazi kwa Jaji Mujulizi, kuwa kunatokana na kashfa ya Escrow, wakisema amesoma alama za nyakati.
Jaji Mujulizi alikuwa ni mmoja wa vigogo waliotajwa kupokea mgawo wa Sh milioni 40.4 kutoka kwa Mwenyekiti wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira, uliotokana na fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Jumla ya Sh bilioni 321 ziliwekwa katika akaunti hiyo na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kusubiri suluhu ya kesi yake na Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Siku chache baada ya kuibuliwa kwa kashfa hiyo, Rugemalira aliyekuwa akimiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL, alisema kati ya fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo, alilipwa Dola za Marekani milioni 75 sawa na Sh bilioni 120  ambazo aliziita ‘vijipesa vya ugoro’.

Share To:
Magpress

MagPress

Vestibulum bibendum felis sit amet dolor auctor molestie. In dignissim eget nibh id dapibus. Fusce et suscipit orci. Aliquam sit amet urna lorem. Duis eu imperdiet nunc, non imperdiet libero.

0 comments so far,add yours