RAIS Dk. John Magufuli ameshtukia mchezo unaofanywa na baadhi ya watu wakiwamo viongozi, kuficha mabilioni ya fedha ndani na kutangaza uamuzi mzito wa kubadili noti mpya ili wakose mahali pa kuzipeleka.
Kutokana na hali hiyo, amewataka watu hao kuzitoa mara moja fedha walizoficha ndani ya majumba yao chini ya magodoro ziingie katika mzunguko ili zikatumike kwenye miradi ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa na Serikali ya awamu ya tano.
Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam katika mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi (ERB), ambao uliwakutanisha wahandisi wa ndani na nje ya nchi ukiwa na lengo la kujadili namna ya kuboresha mazingira ya kazi zao na kutafuta njia sahihi ya kutatua changamoto zao.
Dk. Magufuli alisema kuwa muda wowote anaweza akabadilisha fedha ili wanaozificha fedha hizo za umma wapate hasara kwa kuwa wamesababisha hasara kubwa kwa wananchi.
Alisema fedha nyingi zimepotea katika kulipa wafanyakazi hewa na kulipia miradi hewa ambayo haitekelezeki na tayari ofisi yake imeanza kubaini na kuwafikisha mahakamani, huku akiahidi hakuna mtu atakayeweza kuukwepa mkono wa sheria.
“Kuna mijitu inaficha hela chini ya magodoro na mabenki, ninatamani kubadilisha fedha ili wale wote walioficha ziwaozee huko huko. Katika siku hizi mbili ninaweza kubadilisha fedha na waliozificha wazitoe wenyewe ili ziweze kuingia kwenye mzunguko.
“Na wajiandae hata siku hizi hizi mbili naweza kubadilisha fedha, hii meseji iwafikie wale wanaoficha fedha kwenye magodoro na mabenki,” alisema  Dk. Magufuli.
Alisema fedha za bure bure hazitakuwapo tena. “Kwa sasa watu watapata fedha kwa kufanya kazi na huu ndio wakati wa kutajirika,”alisema Dk. Magufuli.
Akizungumzia changamoto za sekta ya elimu nchini, alisema alipoahidi kutoa elimu bure hakujua idadi ya wanafunzi ambao watapata elimu hiyo.
Alisema katika kipindi cha nyuma walikuwa wanaandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza milioni moja na mwaka huu wameandikisha wanafunzi  milioni mbili, hivyo ongezeko hilo ni changamoto kwa Serikali yake.
“Shule za sekondari wamefanikiwa kupata madawati kwa asilimia 98 na kwa shule za msingi asilimia 88, zoezi la madawati tunakamilisha mwezi huu,” alisema.
Alisema hivi sasa kuna wafanyakazi hewa na wanafunzi hewa. Kwa Mkoa wa Arusha wamebaini wanafunzi hewa 10,000 na Mwanza 8,000.
“Idadi ya wafanyakazi hewa hadi sasa wamefikia 16,500 kwa miaka yote, nawahakikishia bado kuna wafanyakazi hewa, watafikia 20,500… hizo ndiyo changamoto kwangu,” alisema.
Pamoja na hali hiyo alisema kuwa mapato ya Serikali yameongezeka kutoka asilimia 26 hadi 40, na kwamba Septemba 19, wanatarajia kupokea ndege mbili aina ya Jet ambazo zimelipiwa na fedha zilizobaki zipo tayari. Ndege hizo zitatua kwenye viwanja vitatu.
UCHUNGUZI VIWANJA VYA NDEGE
Dk. Magufuli alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha  2016/17, alitenga Sh bilioni 100 kwa ajii ya kutengeneza na kukarabati viwanja vya ndege kwa kiwango cha lami.
“Uwanja wa ndege Dodoma umegharimu shilingi bilioni 11. Kwa bajeti ya bilioni 100, tulitegemea fedha hizo zitatengeneza viwanja vinane. Uwanja wa Mwanza umegharimu shilingi bilioni 105 na upanuzi wa Uwanja wa Dar es Salaam shilingi bilioni 600. Ni kwa nini viwanja viwili vimetumia gharama kubwa hivyo?” alihoji Rais Magufuli.
Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa anataka kufanya uchunguzi ili kuweza kubaini ukubwa huo wa gharama hali ya kuwa waliofanya tathmini ni watu anaowaamini.
Rais Magufuli alisema hivi sasa kuna miradi mingi ya ndani ambayo inatarajiwa kuanza ujenzi wake na kuagiza wapewe wakandarasi wa ndani ambao kama wataamua kufanya kazi, ni wazi nchi itapiga hatua ikiwamo kufikia kuwa na taifa la uchumi wa kati.
“Mchakato wa kutengeneza reli ya kisasa ‘Standard Gauge’ tumetenga zaidi ya shilingi trilioni moja na kuna kutengeneza bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Tanga zaidi ya kilometa 14,000. Je, wahandisi wa Tanzania tumejipanga vipi ili kuhakikisha fedha zinabaki hapa?” alihoji.
USHAURI WA WAHANDISI
Alisema hivi sasa Serikali ipo mbioni kuleta ndege na meli ambazo zinahitaji wahandisi ambapo alihoji ushauri wa wataalamu hao kuhusu vyombo hivyo.
“Wahandisi tujitahidi kuzuia mchanga wetu. Katika vitu vinavyoniuma ni hicho, tumeibiwa mno na tumechezewa mno, kila mahali ni dili, anachukua fedha anatumia anavyo taka,” alisema.
Rais Magufuli alisema Watanzania ni watu wa ajabu na wana kila kitu ikiwamo gesi inayopatikana nchini.
“Nitashangaa sana kwenye uongozi wangu wahandisi kama hamtasaidiana, na katika uteuzi wangu nimependelea wahandisi na nimejitahidi kuwawekaweka kwenye kila eneo. Mnataka nifanyeje wahandisi?” alisema na kuhoji.
Aliwataka wahandisi hao wajitambue, wajipende na kwamba atafurahi siku moja ikiwa wataweza kutengeneza kampuni yao.
“Mbadilike, ‘you need to change’, kila kitu kinahitaji mhandisi au aje malaika kutoka mbinguni ndiyo mtabadilika? Muache wivu mtajenga nchi na msipoamua mtabaki kuwa wasindikizaji,” alisema.
Awali akitoa maelezo kwa Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Bodi ya Wahandisi (ERB), Profesa Ninatubu Lema, alisema hadi sasa idadi ya wahandisi 173,53 nchi nzima wamesajiliwa. Wawili walikuwapo baada ya uhuru.
“Upungufu wa fundi mchundo unasababishwa na kutokuwapo kwa mikopo katika vyuo wanavyosoma  katika ngazi ya stashahada na kukimbilia ngazi  ya shahada kwa sababu  wanapewa mikopo ya kujikimu,” alisema Profesa Lema.
Mwenyekiti huyo wa ERB, alimuomba Rais Magufuli aelekeze miradi yote mikubwa itumike kama darasa la mafunzo kwa wahitimu.
Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa,  alisema sekta ya miundombinu ni muhimu katika kufanya maendeleo.
“Asilimia 59 ya barabara ni kiwango cha lami, lengo kubwa ni kuboresha usafiri wa maji na nchi kavu,” alisema Profesa Mbarawa.

Share To:
Magpress

MagPress

Vestibulum bibendum felis sit amet dolor auctor molestie. In dignissim eget nibh id dapibus. Fusce et suscipit orci. Aliquam sit amet urna lorem. Duis eu imperdiet nunc, non imperdiet libero.

0 comments so far,add yours