Rais Jakaya Kikwete amevitaka vyombo
vya upelelezi kutokukurupuka kwa kupeleka kesi mahakamani ambazo
upelelezi haujakamailika matokeo yake wanashindwa kesi na kwamba huko ni
kumnyima mtu haki kwa kupeleka mashitaka yasiyostahili.
Rais Kikwete ametoa rai hiyo jijini Dar es salaam wakati wa
maadhimisho ya siku ya sheria nchini ambapo amesema watanzania lazima
wapate haki tena kwa wakati na kuwataka mawakili, waendesha mashitaka na
vyombo vya upelelezi kufanyakazi kwa pamoja ili visiwe chanzo cha
kuchelewesha mashauri pasipo sababu na kama shitaka halikamilika
wasikamate watu huku akielezea hatua mbalimbali serikali ilizochukuwa
katika kuboresha mfumo wa mahakama.
Jaji mkuu wa Tanzania Mh Mohamed Chande Othuman amebainisha baadhi
ya vikwazo vinavyochangia kukwamisha ufanikishwaji wa fursa ya wananchi
kupata haki kuwa ni pamoja na sheria nyingi kutokuwa kwenye lugha ya
taifa kwani zimeandikwa kwa lugha ya kiingereza, huku akilitaka bunge
kuangalia namna ya kufanya ili sheria ziwe rafiki kwa watumiaji wote
kwani watanzania wengi wanakosa haki kwa kutokuelewa lugha inayotumika.
Katika hotuba yake mwanasheria mkuu wa serikali Bw George Masaju
amesema mahakama ndiyo kimbilio la watu wanaohitaji haki hivyo ina
wajibu wa kuwasikiliza watu wanaofungua au kufunguliwa mashauri na kutoa
uamuzi kwa kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au
kiuchumi, kutochelewesha haki, kutoa fidia ipasayo kwa watu
wanaoathirika kutokana na makosa ya watu wengine.
Akisoma hotuba ya chama cha wanasheria Tanganyika TLS rais wa chama
hicho Charles Rwechungura amesema uelewa mdogo wa sheria miongoni mwa
wananchi unachangia kuzuia upatikanaji wa haki ambapo ametolea mfano
mkoa wa Dodoma ambako wamebaini kuwa idadi kubwa ya watu walipoteza haki
zao za umiliki wa ardhi na masuala ya ndoa kwa sababu ya kutokujua njia
gani watumie ili kupata haki hadi muda wa ukomo uliowekwa chini ya
sheria ulipomalizika.
0 comments so far,add yours