MWANASIASA mkongwe aliyewahi kuwa swahiba na mshauri mkuu wa Rais Jakaya Kikwete, Kingunge Ngombale Mwiru, ametoa kauli nzito inayoonyesha hakubaliani na msimamo wa Rais Kikwete na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kingunge akimkejeli Rais na chama chake, ambacho yeye ni mmoja wa waasisi, alisema walikurupuka kukubali na kuanzisha mchakato wa Katiba mpya.

Kwa mujibu wa Kingunge, kabla ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza na kuanzisha mchakato wa Katiba mpya, CCM haijawahi kufanya kikao na kuamua kuhusu suala hilo, kama walivyofanya kabla ya mchakato wa kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1991.

Mbali na kumshangaa Kikwete na chama chake, vile vile Kingunge aliwashambulia wazee wenzake wanaounga mkono mapendekezo ya rasimu ya Katiba mpya kuhusu muungano wa serikali tatu.

Katika hali isiyo ya kawaida, Kingunge alisema wazee hao ni “sawa na watu waliochanganyikiwa”.

Anasema msimamo wake unatokana na ukweli kuwa CCM haijawahi kuwa na ajenda ya kuandika Katiba mpya na kwamba ndiyo maana suala hilo halikuwa kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM 2010.

Alisema hoja ya Katiba mpya ni ya wapinzani, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kingunge alisema kimsingi aliyeafikiana na hoja ya wapinzani kuhusu Katiba mpya ni Rais, si CCM.

Kuhusu wazee hao ambao alisema “wamechanganyikiwa” Kingunge alisema anashangaa kuona wazee ni miongoni mwa wanaopendekeza muundo wa serikali tatu, kwani baadhi yao walishiriki katika kuunda mfumo huu uliopo ambao umedumu tangu mwaka 1964.

Alisema muungano wa serikali mbili umeleta mafanikio kwa kujenga udugu na umoja wa kitaifa na kwamba kwa sababu hiyo ungeachwa uendelee badala ya kupiga kelele kwamba ufutwe, ziletwe serikali tatu.

Alisema baadhi ya viongozi wameshindwa kuthamini mafanikio ya muungano na sasa mawazo yao yote yamekuwa yakielekezwa kwenye vyeo vyenye marupurupu.

Aidha alipinga kauli za baadhi ya viongozi wanaosema kuwa kuwepo kwa serikali tatu kutasaidia kuimarisha muungano. Alisema serikali tatu zitaua muungano.

Kingunge aliongeza kuwa kama serikali mbili ni sababu za kufa muungano huo, basi usingeweza kudumu kwa miaka 50 sasa.

“Huu ni mpango wa wakubwa kutaka kujiwekea mazingira ya vyeo, kwani wapo ambao tayari wamekwishajiandaa kuwania urais wa Tanganyika.

“Nilishangaa sana hata huko bungeni watu wanapeana sifa za kuwa fulani anastahili kuwa Rais. Huu ni upotoshaji mkubwa kwa taifa,” alisema, akirejea kauli iliyotolewa juzi na Waziri asiyekuwa na wizara maalumu, Profesa Mark Mwandosya, aliyemfagilia Spika wa Bunge, Anna Makinda, kwamba anafaa kuwa Rais.

Kingunge aliongeza kuwa kwa maoni yake lazima Katiba mpya iweke mipango ya maendeleo ambayo itashirikisha wananchi wa ngazi zote.

Kingunge alisema isiwe mipango hiyo inapangwa na viongozi kutoka juu na kuishusha chini bila kujua wanahitaji nini kabla.

Alisema Katiba inayotakiwa ni ile itakayosimamia na kupatikana kwa maendeleo yanayofanana kati katika jamii.

Kuhusu uraia wa nchi mbili, Kingunge alisema suala hilo lilikuwa linasemwa pembeni lakini sasa wanataka suala liingizwe kwenye Katiba.

“Mwanzo nilijua ni utani lakini nilishangaa suala hili kubwa kuliona limeingizwa kwenye kijitabu kilichotolewa na chama changu na kupendekeza hivyo,” alisema.

Alisema suala la uraia ni la nchi, hivyo chama kilipaswa kutoa nafasi kwa wananchi kujadili kwa kina jambo hilo na sio viongozi kujiamulia wenyewe.

“Kwa mfano nchi yetu ilipovamiwa na Nduli Idd Amini kama kungekuwa na vijana wenye uraia wa nchi mbili wangejiweka upande gani, hii ni mipango ya watu wanaopenda kunogewa na maisha kwenye nchi za watu,” alisema.

Alisema amekuwa kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kwa muda mrefu lakini hakuwahi kusikia hata siku moja kujadiliwa suala hilo ambalo ameliita kuwa la hatari.
Share To:
Magpress

MagPress

Vestibulum bibendum felis sit amet dolor auctor molestie. In dignissim eget nibh id dapibus. Fusce et suscipit orci. Aliquam sit amet urna lorem. Duis eu imperdiet nunc, non imperdiet libero.

0 comments so far,add yours