Freeman Mbowe
*Kamati ya maridhiano kuundwa
*Nia kurejesha umoja, mshikamano
*Lissu, Mnyika wamshangaa Zitto

Zitto Kabwe
UAMUZI wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kumvua madaraka, Zitto Kabwe unadaiwa kuanza kukitesa chama hicho na kwamba sasa uongozi wa juu umeamua kusaka suluhu ya jambo hilo.

Taarifa ambazo RAI Jumatano imezinasa kutoka Kinondoni, jijini Dar es Salaam yalipo Makao Makuu ya Ofisi za Chadema, zinaeleza kuwa, tayari baadhi ya viongozi wamekubali kuketi meza moja ya mazungumzo na Zitto baada ya kupewa ushauri na watu mbalimbali wakiwamo wasomi wakubwa wanaoheshimika ndani ya chama hicho.

Hatua hiyo imekuja wakati ambao tayari uamuzi wa kuwavua madaraka, Zitto pamoja na Mwanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitila Mkumbo, umesababisha mtafaruku na mgawanyiko ndani ya chama.

Uamuzi wa kuwavua uongozi makada hao ambao ulitangazwa na Tundu Lissu mbele ya Freeman Mbowe, ulipokelewa kwa mtazamo tofauti na makada wa chama hicho, ambapo baadhi waliamini kuwa ni sahihi huku wengine wakiyapinga kwa madai kuwa yanaua demokrasia hasa kwa chama ambacho kimejipambanua kupigania demokrasia nchini.

Miongoni mwa makada wanaodaiwa kupingana na hatua hiyo ya kamati kuu ni wasomi, ambapo mmoja wao amemtaka Mbowe kutumia nafasi yake ya uenyekiti kuzungumza na Zitto ili kukinusuru chama.

Msomi huyo aliyebobea katika masuala ya sheria nchini, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, pamoja na kutokubaliana na baadhi ya vitendo vya Zitto, anadaiwa kuweka wazi kwamba utaratibu uliotumika kumuadhibu si sahihi na hivyo ni vema jitihada za haraka zikafanyika ili kulimaliza suala hilo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo kutoka kwenye chanzo cha kuaminika kilicho karibu na Mbowe, mara baada ya kutangazwa kwa maamuzi ya kuwavua uongozi Zitto, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, msomi huyo alizungumza kwa kina na Mwenyekiti wake na inaelezwa kuwa baadhi ya maneno mazito aliyotumia kumfikishia ujumbe yalisababisha Mbowe amwage machozi.

“Mwenyekiti alilia baada ya kuelezwa maneno mazito na mmoja wa wanasheria wa chama, alimtaka aachane na mivutano hii na badala yake akae mezani na Zitto ili wayamalize,” alisema mtoa habari wetu.

Imeelezwa kuwa baada ya ushauri huo, Mbowe alimuomba mwanasheria huyo kumtafuta, Zitto ili wakae mezani.

Imebainika kwamba ni suala gumu kwa Mbowe kukaa meza moja na Zitto bila ya kuwepo kwa mtu wa kuwasuluhisha kutokana na wawili hao kuwa na migogoro iliyodumu kwa muda mrefu.

Katika kuhakikisha Mbowe na Zitto wanakutana na wanamaliza tofauti zao zilizoanza kuchomoza mwaka 2009, tayari kuna mipango ya kuunda Kamati ya usuluhishi ambayo inatajwa huenda ikaongozwa na Profesa Mwesigwa Baregu na Mabere Marando.

Jukumu la wateule hao ni kuhakikisha wanawakutanisha mahasimu hao ili kurejesha umoja na amani ndani ya chama.

Aidha zipo taarifa kwamba katika kuhakikisha amani ya moja kwa moja inarejea ndani ya chama, Zitto amepangiwa kupewa nafasi ya kuwania umakamu Mwenyekiti Bara, huku Mbowe akiachiwa nafasi yake.

Mbali na kuachiwa nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti, pia zipo taarifa kwamba Zitto ataachiwa jukumu la kuwania nafasi ya urais kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, wakati ambapo mwaka 2015, Dk. Willbrod Slaa atawania nafasi hiyo kwa mara ya pili.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa, Profesa Baregu na Marando wamepewa jukumu hilo la kusuluhisha, kutokana na ushawishi walionao kwa pande zote mbili.

Inaelezwa kuwa Profesa Baregu amekuwa ni muumini wa demokrasia ya kweli ndani ya chama na kwamba hakukubaliana na maamuzi ya kumvua uongozi Zitto na Dk. Kitila na ndiyo sababu iliyomchagiza kutaka kujiuzulu nafasi yake ya ujumbe wa Mkutano Mkuu.

Profesa Baregu, Said Arfi ambaye amejiuzulu nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho na Dk. Kitila Mkumbo ni miongoni mwa makada wanaoaminika kusimamia demokrasia ya kweli ndani ya chama.

Msemaji wa Chadema, John Mnyika alipotafutwa kuzungumzia taarifa hizo, hakukubali wala kukataa badala yake alisema masuala hayo hayajui.

Kwa upande wake, Zitto ambaye kwa sasa yuko nchini Uingereza kwa kazi za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), aliliambia Rai Jumatano kwamba taarifa hizo za chama kusaka suluhu naye amezisikia na endapo atatakiwa kufanya hivyo haoni sababu ya kukataa.

“Nia yangu ni kuona tunavuka salama kwenye upepo huu na ndio maana nimetangaza kwamba sitoki Chadema, njia pekee ya kuyamaliza haya ni kuzungumza, sidhani kama nitakuwa na kipingamizi,” alisema Zitto.

Kwa upande mwingine jana chama hicho kimewaandikia barua yenye mashitaka 11, Zitto, Mwigamba na Dk. Kitila.

Mbali na mashitaka hayo, pia katika barua hizo, wamepewa muda wa siku 14 kujieleza kimaandishi ni kwanini wasichukuliwe hatua za zaidi, kabla ya kujitetea tena mbele ya Kamati Kuu ya chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, Mnyika, alisema sekretarieti iliyokutana juzi, ilikamilisha uamuzi uliopitishwa na Kamati Kuu ya kuwavua nyadhifa zao ndani ya chama.

Alisema sekretarieti ilijiridhisha kuwa makosa yao yalitokana na waraka ambao kimsingi ulikiuka kanuni, maadili na taratibu za chama.

“Mashitaka na makosa 11 waliyofanya, yamejikita katika uamuzi wa Kamati Kuu na si maneno ambayo waliyazungumza mbele ya waandishi wa habari katika mkutano wao wa Jumapili.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu, alisema Zitto na wenzake wasipojieleza ndani ya siku 14, taratibu ambazo hakuzitaja zitafuatwa.

Aidha, alimshangaa Zitto kupoteza lengo kwa kuwaambia waandishi wa habari kuwa amefukuzwa kwa sababu za uongo na kwamba ni za kizushi.

“Walichokifanya ni kupoteza lengo kwamba wamefukuzwa kwa masuala ya PAC (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali), posho za vikao vya Bunge, kuuza majimbo yetu ya uchaguzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na mambo mengine waliyoyataja.

“Wamefukuzwa kwa kufanya mapinduzi bila kufuata utaratibu, yaani kwa kifupi walikiuka maadili, hata hivyo, katika mashitaka yao hayakuzungumzia habari za PAC,” alisema Lissu.

Kuhusu kauli ya Wakili wa Zitto, Albert Msendo, kwamba Kamati Kuu ilijivika mamlaka yasiyoihusu kuwavua nyadhifa zao, isipokuwa Baraza Kuu, Lissu alisema Kamati Kuu ilikuwa sahihi kuchukua uamuzi ule.

Kuhusu kauli ya Zitto kwamba ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu ndani ya Chadema, alisema si kweli kwani haiwezekani amtukane Mwenyekiti (Freeman Mbowe), kisha aseme anaheshimu chama.

Aidha Chadema imesema waraka uliosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kuchapishwa na baadhi ya magazeti ni feki, na kwamba waraka halisi wanao na watautoa kwenye mitandao wakati ukifika.

HISTORIA YA MGOGORO WA ZITTO NA MBOWE

Historia ya mgogoro wa Zitto na Mbowe inaanzia mwaka 2009, wakati Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini alipoamua kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya uenyekiti kwa staili ya kumshtukiza Mbowe ambaye alikuwa akiwania kwa awamu ya pili.

Mbowe alichukua nafasi hiyo mwaka 2004 kutoka kwa marehemu Bob Makani, ambaye alikiongoza chama hicho kwa awamu moja kutoka mwaka 1998 hadi 2004, kama alivyofanya mtangulizi wake, Edwin Mtei ambaye ndiye mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho aliyekiongoza kutoka mwaka 1993 hadi 1998.

Katika kipindi cha awamu ya kwanza Mbowe alifanikiwa kuimarisha harakati za chama hicho, ambapo aliweza kuongeza idadi ya wabunge kutoka sita walioachwa na Makani hadi kufikia 11, watano wakiwa ni wa kuchaguliwa na sita wa kuteuliwa.

Hatua hiyo ilimpa hamasa mwenyekiti huyo kukiongoza zaidi chama, ambapo mwaka 2009 wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani, alionesha dhahiri kukataa kupingwa kwenye uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Kiramuu, jijini Dar es Salaam.

Maamuzi ya Zitto kujitosa kuwania nafasi hiyo ya uenyekiti, yaliibua msuguano mkali kati yake na Mbowe aliyekuwa akiungwa mkono na muasisi wa chama hicho, Mtei pamoja na baadhi ya makada waliokuwa na dhana kwamba Mwenyekiti huyo hastahili kupingwa.

Hofu ya Mbowe kupingwa ilizalisha makundi ndani ya chama, ambapo kundi la mwenyekiti huyo lilimuona Zitto ni mtovu wa nidhamu na hamuheshimu kiongozi wake na kwamba hakustahili kumpinga mtu ambaye hajamaliza muhula wake wa pili wa uongozi ndani ya chama.

Wanamtandao wa Mbowe wakaibua hoja kwamba ni vema Zitto akaondoa jina lake kwenye kuwania nafasi hiyo, ili kukiepusha chama na anguko wakati huo kikijiandaa kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kwamba kama chama kingeingia kwenye uchaguzi na mgawanyiko hali ingekuwa mbaya.

Jitihada za haraka za kukinusuru chama na mpasuko zikafanyika, ikiwa ni pamoja na kufanya kikao cha usuluhishi kilichoundwa na wazee kwa nia ya kutafuta muafaka kati ya Zitto na Mbowe, mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini alishawishiwa kuliondoa jina lake kwenye kinyang’anyiro hicho.

Hatua hiyo ilififisha dhana ya uwepo wa demokrasia na badala yake ukawa mwanzo wa kuzaliwa kwa makundi.
Share To:
Magpress

MagPress

Vestibulum bibendum felis sit amet dolor auctor molestie. In dignissim eget nibh id dapibus. Fusce et suscipit orci. Aliquam sit amet urna lorem. Duis eu imperdiet nunc, non imperdiet libero.

0 comments so far,add yours