Na RAPHAEL OKELLO, BUNDA
MKAZI wa Kijiji cha Ligamba B wilayani Bunda mkoani Mara, Monica Fumbuka (70), ambaye ni mjane, amechapwa viboko hadharani na kutakiwa kuhama kijijini hapo kwa tuhuma ya wizi.
Akizungumza juzi kwa lugha ya Kisukuma na kutafsiriwa kwa Kiswahili  kwa  waandishi  wa habari na mmoja wa binti zake Sikitu Girya nje ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Fumbuka alisema hafahamu sababu za kutuhumiwa kuwa mwizi katika hali ya uzee aliyonayo.
Alisema muda wote alikuwa akiishi vizuri na wanakijiji hao na hafahamu nini kimetokea hadi kufikia hatua ya kutakiwa kuhama katika kijiji hicho na kuacha mali zake, ikiwa ni pamoja na mashamba aliyoachiwa na marehemu mume wake, Thomas Tito aliyefariki mwaka 2009.
“Mimi nilishtuka wanakijiji wanapiga yowe kuelekea nyumbani kwangu, wakanikamata kisha kunipeleka eneo la mkutano wakinituhumu kuwa nimeiba Sh 100,000. Walinichapa viboko na kunitaka nihame kijijini, kisha baadae walinipeleka Kituo Kikuu cha Polisi cha Bunda.
“Wakati napigwa viboko hakujitokeza mwanakijiji yeyote wa kunitetea na baada ya kunitoa polisi  walinipeleka mahakamani   na kutakiwa kulipa kiasi cha Sh 150,000,” alisema Fumbuka.
Akizungumza juzi katika mkutano uliowahusisha wenyeviti wa mitaa, vijiji, watendaji wa kata na vijiji pamoja na Kamati ya Ulinzi  na Usalama wa Wilaya ya Bunda, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ligamba B, Charles Gedi, alikiri  kufanyika kwa mkutano aliouita ‘yowe’ katika kijiji hicho uliomtuhumu bibi huyo kwa wizi na kutakiwa kukihama kijiji hicho.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili,  alisema haridhishwi na uamuzi huo uliofanywa na mikutano  ya ‘yowe’  na kusema unakiuka na kuvunja haki za binadamu.
Bupilipili ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, alisema maamuzi mengi yanayotolewa na mikutano ya ‘yowe’ iliyoanzishwa katika vijiji na mitaa ya wilaya hiyo, yanawakandamiza sana wanawake, hivyo kamwe hataweza kuunga mkono mambo hayo.
Share To:
Magpress

MagPress

Vestibulum bibendum felis sit amet dolor auctor molestie. In dignissim eget nibh id dapibus. Fusce et suscipit orci. Aliquam sit amet urna lorem. Duis eu imperdiet nunc, non imperdiet libero.

0 comments so far,add yours