
Wagonjwa wanaohitaji rufaa ya matibabu ya dharura kutoka katika vijiji mbalimbali vya kata za nyanguge, Kisesa na Lugeye wilayani Magu, wako kwenye hatari ya kupoteza maisha yao kufuatia mgomo wa madereva wa magari ya kubeba wagonjwa unaoendelea endapo hatua za haraka hazitachukuliwa na uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kuwalipa fedha zao za uhamisho kiasi cha shilingi milioni tano.
Madereva wa magari ya wagonjwa waliogoma kuhamia kwenye vituo vyao 
vipya ni Andrew Kitalagwa, aliyehamishiwa kituo cha afya Nyanguge, 
Mohamed Bakari aliyehamishiwa Kisesa na Jackson Saguda ambaye amepangiwa
 kazi  katika kituo cha afya Lugeye, madereva hao walihamishiwa kwenye 
vituo hivyo tangu machi 19 mwaka huu lakini hadi sasa bado hawajaripoti 
kazini, jambo ambalo limewasikitisha madiwani wa halmashauri ya wilaya 
hiyo.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Magu Yesse 
Kanyuma akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri 
ya wilaya hiyo amewataka madereva hao kurudi kazini mara moja wakati 
madai yao yakiendelea kushughulikiwa ili kuokoa maisha ya wagonjwa 
wanaoteseka kwa kukosa matibabu ya dharura.

0 comments so far,add yours