
Baadhi ya Wafanyabiashara wa kati Mjini Morogoro wamefunga maduka yao kwa hofu ya kufungiwa na Mamlaka ya mapato nchini TRA na kutozwa mamilioni ya fedha kama faini kutokana na kutokuwa na mashine za risiti za kielektroniki za (EFD) ,wakidai hatua hizo zimeanza kuchukuliwa jijini Dar es salaam, huku bado mazungumzo kati ya TRA na wafanyabiashara yakiwa bado hayajakamilika.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa kati mjini 
Morogoro, Ali Mamba amesema mgomo huo  hauhusiani na matumizi ya mashine
 hizo bali mfumo mzima wa ulipaji wa kodi kwa wafanyabiashara ambao 
pamoja na kushawishiwa kuachana na mgomo huo, wamedaai kuchukua uamuzi 
huo kwa  kutowaamini viongozi  wao katika mazungumzo yaliyokuwa 
yakiendelea baina yao na TRA, kwa kushuhudia mamlaka hiyo ikianza 
kuwafungia wafanyabiashara jijini Dar es salaam.
Kufungwa huko amesema kunakwenda  sambamba na 
masharti  magumu  ikiwemo kutakiwa kulipa faini ya sh milioni tatu, 
kununua mashine kwa laki sita na shilingi elfu themanini ya kufuli 
linalotumika kufungia eneo husika linalofungiwa.
Nao wafanyabiashara wanaosambaza bidhaa katika 
maduka mbalimbali, walieleza kuathiriwa na mgomo huo na kwamba pamoja na
 kutumia mashine husika, bado mtandao wake ni wa tabu, hivyo TRA badala 
ya kutaka wafanyabiashara watumie mashine ni vyema ikaangalia pia na 
changamoto zilizopo kwenye mfumo huo kabla ya kuhimiza matumizi.
Meneja wa TRA mkoa wa Morogoro Kilomba Kanse, 
alikataa kuzungumzia hali hiyo kwa  madai tayari Kamishna mkuu wa 
mamlaka hiyo, Risherd Bade,alishazungumza na vyombo vya habari kuhusiana
 na mashine hizo.
Akinukuliwa na vyombo vya habari, Kamishna Mkuu wa 
Tra, Risherd Bade,mbali na kuzungumzia umuhimu wa  uanzishwaji wa 
mashine za EFD, na kuwahimiza wananchi kudai risiti sahihi kwa kiwango 
cha fedha wanachotoa wanunuapo bidhaa, amewaonya wanaohamasisha, 
kutishia au kutumia njia yoyote kuwarubuni wengine wasitumie mashine 
hizo ama kufunga biashara zao waache mara moja, vinginevyo sheria 
itachukua mkondo wake.
0 comments so far,add yours