WIKI hii, kwa mara nyingine Bunge limeandika historia ya kuwang’oa mawaziri wanne, baada ya kamati yake ndogo kuwasilisha ripoti ya athari zilizojitokeza wakati wa Operesheni Tokomeza Majangili.

Ripoti hiyo, ambayo iliandaliwa na kamati ndogo ya Bunge, ilipewa jukumu la kufanya uchunguzi juu ya athari za Operesheni Tokomeza Ujangili, baada ya kuwapo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kwamba operesheni hiyo imekiuka haki za binadamu, kutokana na watekelezaji wake kusababisha vifo vya watu na mifugo, udhalilishaji pamoja na utesaji.

Madai hayo ya wananchi yalisababisha operesheni hiyo isimame ili kupisha uchunguzi wa kamati ndogo ya Bunge.

Baada ya kamati hiyo ndogo ya Bunge kuwasilisha ripoti yake bungeni juzi, ikieleza uhalisia wa jinsi Operesheni hiyo ilivyofanyika, iliamsha hisia na hasira kali kwa wabunge, ambao walishinikiza mawaziri ambao wizara zao zilitajwa moja kwa moja kuhusika na operesheni hiyo, wajipime kama wanafaa kuendelea kukalia viti vyao.

Baada ya shinikizo hilo kuwa kubwa, kiasi cha kulazimisha Kamati ya Uongozi ya Bunge kukutana na kujadili jambo hilo, vile vile ile ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi, ilimlazimu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, awasiliane na Rais Kikwete, ambaye naye bila shaka akatoa uamuzi wa kutengua uteuzi wa mawaziri wanne, ambao kwa mujibu wa ripoti, wizara zao ndizo zimehusika na mabaya dhidi ya wananchi.

Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Mathayo David pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.

Sisi RAI Jumapili tunaamini kuwa kutenguliwa kwa uteuzi wa mawaziri hao ni fundisho kwa mawaziri waliobaki, kwamba dhamana waliyopewa kusimamia wizara wasiichukulie kama dhamana ya kufanya wanayoyataka wao bila kuangalia maslahi ya Watanzania na taifa.

Ni ukweli ulio wazi kwamba, baadhi ya mawaziri wamekuwa wakitumia siasa kama ngao ya kujikinga na utendaji wao wa kila siku.

Wengine wamejisahau na kujiona kwamba wao ni wa ngazi nyingine na hivyo kuwa wazito kushuka katika ngazi ya chini kuangalia utendaji kazi wao unapokewa vipi na wananchi.

Mawaziri wengi wanafanya kazi kwa mazoea, ni hatua hiyo ndiyo ambayo imesababisha mara kadhaa mambo mengi kwenda kinyume cha malengo ya serikali, ambapo matokeo yake serikali inaonekana haifanyi lolote kwa jamii.

Sisi RAI Jumapili tunakumbusha mawaziri watakaoteuliwa kwamba uamuzi uliowafika mawaziri wanne uwe fundisho kwao na pia utumike kama alama za kusoma nyakati kwa kujipima kama wanaweza kwenda sanjari na mwendokasi unaotakiwa.

Uamuzi huu wa Rais pia ni vyema ukatumiwa kama chachu kwa mawaziri na watendaji wengine wote kukubali kuwajibika kabla ya kuwajibishwa.

Pia tunachukua nafasi hii kuishauri serikali kwamba uamuzi kama huo usikomee kwa mawaziri tu, bali hata kwa watendaji na askari wengine wote walioshiriki kutenda unyama dhidi ya wananchi wakati wa Operesheni Tokomeza.

Tunasisitiza sheria kufuatwa, ili wahusika wabainike haraka na haki iweze kutendeka mara moja.
Share To:
Magpress

MagPress

Vestibulum bibendum felis sit amet dolor auctor molestie. In dignissim eget nibh id dapibus. Fusce et suscipit orci. Aliquam sit amet urna lorem. Duis eu imperdiet nunc, non imperdiet libero.

0 comments so far,add yours