Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inapenda kuwatahadharisha  waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2016/2017
 na umma kwa ujumla kuwa imepokea taarifa kuwa kuna watu wasio waaminifu
 ambao si watumishi wa Bodi ambao huwapigia simu baadhi ya waombaji kwa 
lengo la kuwatapeli.
Taarifa hizo za kitapeli zimekuwa 
zikisambazwa katika siku za hivi karibuni kupitia mitandao mbalimbali ya
 kijamii zikiwataka baadhi ya waombaji wa mikopo au wadhamini wao kutuma
 fedha (Tshs 39,000/-) kwa namba ya simu 0716463190
 ili fomu zao za maombi ya mikopo zilizowasilishwa Bodi zirekebishwe kwa
 kuwa zimeonekana zina makosa na hivyo hawatapata mikopo.
Namba inayotumika kusambaza taarifa hiyo au kupiga simu kutoa taarifa hizo ni 0764640325 na mtu anayepiga anajitambulisha kwa jina la Charles Amos.
Bodi ya Mikopo inapenda kuwataarifu wadau wake wote, wakiwemo wale walioomba mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2016/2017 kuwa taarifa hizo si za kweli. Mtu huyo ni tapeli na si mtumishi wa Bodi ya Mikopo.
Iwapo waombaji watapigiwa simu na matapeli hao, watoe taarifa kwa vyombo vya dola kwa hatua zaidi.
Aidha, Bodi ya Mikopo inapenda 
kuwataarifu waombaji wa mikopo kuwa utaratibu wa Bodi kuwasiliana na 
waombaji wa mikopo ambao fomu zao za maombi hubainika kuwa na upungufu 
haujabadilika. Mara baada ya kazi ya ukaguzi wa fomu kukamilika, Bodi ya
 Mikopo itatoa taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari, ikiwemo 
tovuti hii ya Bodi na kuwaalika waombaji kufanya marekebisho.


0 comments so far,add yours