Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakitia saini Rasimu ya Pili ya Katiba juzi. Rasimu hiyo itakabidhiwa leo kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais Ali Mohamed Shein, Karimjee, Dar es Salaam. Picha ya mtandao.
Dar es Salaam. Swali la nini kilichomo katika Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya litajibiwa leo wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapokabidhi rasimu hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Rasimu inayosubiriwa kwa hamu na wananchi wa kada 
zote itatolewa ikiwa imepita miezi saba tangu tume hiyo ilipotoa Rasimu 
ya Kwanza ya Katiba ambayo ilijadiliwa na kuboreshwa katika Mabaraza ya 
Katiba yaliyoketi kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2, mwaka huu.
Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 3, 2012 kwa kukusanya maoni ya wananchi, iliandaa rasimu ya kwanza iliyotangazwa Juni 4, mwaka huu.
Hafla ya kukabidhi rasimu hiyo itafanyika leo saa 
6.00 mchana katika Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam na 
kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na asasi
 mbalimbali.
Baada ya kukabidhi rasimu hiyo ya Katiba, Tume ya Mabadiliko ya Katiba itavunjwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Warioba 
ndiye atakayesoma rasimu hiyo kwenye Bunge Maalumu la Katiba 
linalotazamiwa kuanza vikao vyake Februari, mwakani.
Alipoulizwa nini kilichoongezwa au kupunguzwa 
katika rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema: “Siwezi kueleza kama kuna 
kilichoondolewa au kurekebishwa... kesho (leo), Watanzania watapata 
fursa ya kujua mapendekezo ya tume, wasubiri.”
Baadhi ya mambo yanayosubiriwa kwa hamu kujua kama
 yamefanyiwa marekebisho au la kwenye Rasimu Mpya ni pamoja na mfumo na 
muundo wa Muungano, umri wa kugombea urais, wabunge kutokana na mikoa, 
umri wa kugombea urais na mengine.
Serikali Tatu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupitia Rasimu ya 
Kwanza ilipendekeza kuundwa kwa Serikali Tatu na alipokuwa akizungumzia 
hilo wakati akitangaza Rasimu ya Kwanza, Jaji Warioba alisema uamuzi huo
 ulifikiwa kwa kuwa yalikuwa ni maoni ya wananchi walio wengi.
Hata hivyo, pendekezo hilo lilizua mjadala mkubwa 
kwani chama tawala, CCM, kilipinga na kuweka bayana kwamba kinataka 
muundo wa Muungano uendelee kuwa wa Serikali mbili.
Vyama vya upinzani kwa upande wake, viliunga mkono
 pendekezo hilo la muundo wa Serikali Tatu huku CUF kikienda mbali zaidi
 kwa kutaka Zanzibar ipewe mamlaka ya kuwa na dola kamili.

0 comments so far,add yours