Madiwani CCM kutua CHADEMA
MBOWE AWAKARIBISHA, AWAPA MBINU
MADIWANI wanane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Kagera waliofukuzwa uanachama wiki iliyopita wamekaribishwa kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ndiye aliyewakaribisha madiwani hao wanaosubiri kufukuzwa rasmi na vikao vya Kamati Kuu ya CCM, vinavyotarajiwa kufanyika wiki hii mkoani Dodoma. Madiwani waliofukuzwa na kata zao kwenye mabano ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni naibu meya (Buhembe), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya (Kashai), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).
        Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Uhuru wa 
Bukoba Mjini, Mbowe alisema CCM imewachakachua madiwani hao wanane na 
hata wakibaki huko chama chao hakitawaona wa maana, kwa sababu chama 
hicho kinalea ufisadi. Mbowe alisema CHADEMA wako tayari kuwapokea 
madiwani hao waliofukuzwa na kuwafundisha siasa za mageuzi. “Tutasimama 
nao katika kujenga Bukoba mpya isiyo na ufisadi kama unaofanywa na Meya 
wa manispaa hiyo iwapo wataamua kuja kwetu, milango ipo wazi 
nawakaribisha,” alisema. Mbowe alisema CHADEMA kinamuunga mkono Mbunge 
wa Bukoba Mjini, Balozi Hamis Kagasheki (CCM), anayepinga ufisadi 
unaofanywa na meya kutoka chama chake, Anatory Amani.

0 comments so far,add yours